Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kongamano hilo la kimataifa linatarajiwa kufanyika siku ya Jumapili, tarehe 10 Mei 2026, katika eneo la Kigamboni – Chadibwa, jijini Dar es Salaam, likiwa limekusanya waumini, wasomi na wadau wa elimu ya Kiislamu kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Tukio hili adhimu linatajwa kuwa moja ya majukwaa muhimu yanayokuza uelewa sahihi wa mafundisho ya Qur’ani Tukufu pamoja na kuimarisha umoja na undugu miongoni mwa Waislamu. Kupitia kongamano hili, washiriki watapata fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kushuhudia vipaji vya hali ya juu vya usomaji wa Qur’ani vinavyovuka mipaka ya kitaifa.
Miongoni mwa wageni mashuhuri watakaolipamba kongamano hilo ni wasomaji wazawa kutoka Tanzania, wakiwemo Eidd Shabani na Rajai Ayubu, wanaotambulika kwa sauti zao zenye mvuto na umahiri mkubwa katika usomaji wa Qur’ani. Kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran watakuwepo wasomaji mahiri kama vile; Moqadami Karim na Muhammadreza Pursafari, huku Pakistan ikiwakilishwa na msomaji mashuhuri Sayyid Mortaza Rizvi, ambaye anasifika kimataifa kwa umahiri wake wa kipekee.
Waandalizi wa kongamano hilo wameeleza kuwa; maandalizi yamekamilika kwa kiwango cha hali ya juu, yakilenga kuhakikisha tukio hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa na kuacha alama ya kipekee kwa washiriki wote. Aidha, wamewahimiza waumini na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hilo la kiroho na kielimu.
Kwa hakika, Kongamano la 31 la Kimataifa la Qur’ani Tukufu linatarajiwa kuwa chemchemi ya nuru, maarifa na mshikamano, likiimarisha zaidi nafasi ya Tanzania katika ramani ya kimataifa ya kukuza na kuhifadhi mafundisho ya Qur’ani Tukufu. Ni tukio lisilopaswa kukosa kuhudhuriwa na kila mwenye kiu ya elimu na mapenzi kwa Kitabu Kitakatifu.
Maoni yako